WATUHUMIWA watatu wa
ujambazi wameuawa baada
ya kurushiana risasi na polisi
katika eneo la Igogo jijini
Mwanza, katika jaribio la
kuvamia Kituo cha Mafuta
cha GBP.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Mwanza, Ernest Mangu,
alisema jaribio hilo lilifanyika
juzi kati ya saa 2 na 3 usiku,
katika kituo hicho cha
mafuta kilichopo katika
barabara ya Kenyata.
Alisema majambazi ambao
idadi yake haikufahamika
mara moja, baada ya
majibizano ya risasi na polisi,
wengine walitoroka lakini
askari Polisi walifanikiwa
kukamata bunduki moja
aina ya SMG, yenye namba ya
usajili 2916 pamoja na risasi
saba.
Akifafanua, Mangu alisema
walipokea taarifa kutoka
kwa raia wema juu ya
kuwepo kwa majambazi
kutoka Ngara yaliyopanga
njama ya kuvamia kituo
hicho cha mafuta.
Alisema majambazi hayo
yalipofika katika eneo la
tukio na kujiandaa kuvamia
kituoni hapo, polisi nao
walijitokeza, ndipo
walipoanza kurushiana
risasi na majambazi hao,
ambapo watuhumiwa
watatu waliuawa huku
wengine wakitokomea
kusikojulikana.
Katika eneo la tukio kwa
mujibu wa Kamanda Mangu,
yaliokotwa maganda ya
risasi 22 huku miili ya
watuhumiwa ikihifadhiwa
katika Hospitali ya Rufaa ya
Bugando na Polisi mkoani
hapa linaendelea na
uchunguzi.
Kamanda Mangu ametoa
mwito kwa wananchi
kuendelea kutoa taarifa za
siri kwa jeshi hilo, ili lizuie
matukio ya uhalifu.
Katika tukio lingine, watu
wasiojulikana wameteketeza
kwa moto nyumba tisa za
nyasi za familia moja katika
kijiji cha Nyehunge wilayani
Sengerema mkoani hapa.
No comments:
Post a Comment