Tuesday, August 13, 2013

MAJAJI WATATU KUSIKILIZA KESI YA WAZIRI MKUU

Mahakama Kuu Kanda ya Dar
es Salaam, likiongozwa na
Jaji Kiongozi Fakhi Jundu
linatarajia kusikiliza kesi ya
kikatiba inayomkabili Waziri
Mkuu Mizengo Pinda.
Kesi hiyo ilifunguliwa Agosti
mosi mwaka huu na Kituo
cha Sheria na Haki za
Binadamu (LHRC), wakipinga
kauli ya Waziri Pinda
aliyoitoa bungeni hivi
karibuni kwamba
wanaokaidi maagizo ya Dola,
wapigwe.
Kwa mujibu wa taarifa
iliyopatikana mahakamani
hapo, mbali na Jaji Kiongozi,
majaji wengine
watakaosikiliza kesi hiyo
inayomkabili Waziri Pinda
pamoja na Mwanasheria
Mkuu wa Serikali (AG), ni Jaji
Augustine Mwarija na Dk
Fauz Twaib.
Inadaiwa Mei 20 mwaka
huu, Pinda akiwa bungeni
katika nafasi yake ya Waziri
Mkuu, kinyume na Katiba ya
Nchi alitoa kauli ya kuruhusu
askari wa Jeshi la Polisi
kuwapiga raia ambao
hawatatii amri yao
kunapokuwa na vurugu.
“Sasa kama wewe umekaidi,
hutaki, unaona kwamba ni
imara zaidi, wewe ndio jeuri
zaidi watakupiga tuu na
mimi nasema muwapige tu
kwa sababu hakuna namna
nyingine, eeh maana
tumechoka sasa,” sehemu ya
hati ya mashitaka iliyonukuu
kauli ya Waziri Pinda.
Katika hati hiyo inadaiwa
kwa mujibu wa utekelezaji
wa Sheria za Jinai, kauli
inayotolewa na kiongozi wa
nafasi ya Waziri Mkuu,
inaonekana kama amri
inayopaswa kutekelezwa na
vyombo vya Dola kama Polisi,
hivyo itachukuliwa kama
amri halali na kusababisha
waendelee kuwatesa na
kuwapiga wananchi wasio
na hatia.
Aidha inadaiwa Pinda
alivunja ibara ya 100 ya
Katiba inayompa kinga
mbunge anapotoa jambo
lolote bungeni, kwa kuwa
yeye hakuzungumza
bungeni kama mbunge, bali
alikuwa anatoa msimamo
wa Serikali yake.
Akizungumza hivi karibuni,
Mkurugenzi wa Mashitaka
(DPP) alisema hakuna uhalali
wa mashitaka hayo kwa
sababu kauli ya Pinda kuwa
pigeni haikuwa piga ua,
alichosema ni kupiga wale
wasiotaka kutekeleza amri
halali.
Alifafanua kuna sheria ya
kutumia nguvu pale ambako
kuna mkusanyiko usiokuwa
wa halali pindi raia
wanapokaidi kutawanyika
kwa hiari hivyo hakuna
shaka kauli ya Waziri Mkuu
ililenga hivyo.

No comments:

Post a Comment