Baraza la waisilamu Tanzania
limeunga mkono kauli ya
Jumuiya ya taasisi za kisilamu za
kuitaka serikali kuchunguza kwa
kina tukio lililopelekea kupigwa
risasasi kwa mhubiri wa
kiisilamu Sheikh Issa Ponda.
Taarifa imetolewa na kaimu
mufti wa Tanzania Al Had Musa
Salum.
Pamoja ya kwamba (BAKWATA)
limekuwa likipingana na
misimamo ya Sheikh Ponda
limesema serikali ilikuwa na
nafasi ya kumkamata Ponda kwa
kufuata mkondo wa sheria.
Kwa mujibu wa mwandishi wa
BBC mjini Dar es Salaam, Baruan
Muhuza, sheikh huyo ambaye
amekuwa katika mivutano ya
mara kwa mara na serikali ya
nchi hiyo alipigwa risasi baada
ya kutokea vurugu kwenye
mkutano wa mawaidha ya
baraza la sikukuu ya Idd el Fitr.
Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo,
Alhajj Mussa Kundecha,
amewaambia waandishi wa
habari mjini humo kuwa endapo
serikali haitachukua hatua
itakayowaridhisha Waislamu,
wataamua kufikiria upya
mustakabali wao na serikali ya
Tanzania.
Sheikh Ponda amelazwa katika
hospitali ya taifa, Muhimbili, mjini
Dar es Salaam akiuguza jeraha la
risasi huku akiwa chini ya ulinzi
wa askari kanzu.
Msemaji wa Jeshi la polisi nchini
humo Advera Senso ameiambia
BBC mjini Dar es Salaam kuwa
jeshi lake kwa kushirikiana na
jukwaa la haki jinai wameunda
kikosi kazi kwa ajili ya kufanya
uchunguzi wa tukio hilo huku
akikana kuwa Sheikh Ponda
alipigwa risasi na polisi.
Senso amewalaumu wafuasi wa
Sheikh Ponda kwa kuwazuia
askari kumkamata Sheikh huyo
kwa kuwarushia mawe; hatua
iliyosababisha askari hao
kufyatua risasi hewani ili
kuwatawanya na hata hivyo
wafuasi hao walifanikiwa
kumtorosha kiongozi huyo wa
kidini.
Taarifa za jumuiya hiyo ambayo
inajulikana zaidi Tanzania kama
Shura ya Maimamu zinasema
kuwa Sheikh Ponda ambaye
polisi wanasema walikuwa
wakimtafuta kwa tuhuma za
kutoa matamko ya uchochezi,
alisafirishwa usiku kutoka mji wa
Morogoro hadi Dar es Salaam
zaidi ya kilomita 200.
Sheikh Ponda kwa sasa
anatumikia kifungo cha nje cha
mwaka mmoja alichohukumiwa
mapema mwaka huu baada ya
kukutwa na makosa kadhaa
ikiwemo uchochezi wa kuharibu
mali za watu.
No comments:
Post a Comment