Thursday, August 8, 2013

MAHABUSU WAGOMA ARUSHA

MAHABUSU wanaokabiliwa
na kesi mbalimbali zikiwemo
za mauaji, ubakaji na
unyang’anyi, katika gereza
kuu la Kisongo mkoani
Arusha, wamegoma kushuka
kwenye karandinga muda
mfupi baada ya kufikishwa
mahakamani, wakimtaka Jaji
Mkuu Mohamed Chande
Othman, awasikilie kero zao.
Mgomo huo ulifanyika jana
asubuhi saa 2.50 na kudumu
kwa takribani dakila 15 , hali
iliyolazimu shughuli za
Mahakama kusimama kwa
muda kutokana na kelele za
mahabusu hao na nyimbo
mbalimbali, walizokuwa
wakiimba wakidai
wamechoka kunyanyaswa
na wanachohitaji ni haki.
Mahabusu hao wakiwa
kwenye Basi la Magereza
lenye namba MT 0047,
walisikika wakidai
kunyanyaswa na askari
magereza, kubambikiwa
kesi, kesi zao
kucheleweshwa na kwamba
wanamtaka Jaji Mkuu afike
kusikiliza kero zao.
Baadhi walidai wamekaa
gerezani kwa muda mrefu
bila kesi zao kusikilizwa,
huku wengine wenye kesi
kama zao wakifika muda
mfupi na kesi zao kutajwa
na kuanza kusikiliza na
kutolewa uamuzi.
Waliwatuhumu
wamepelelezi wa kesi wa
wilaya (OC CID) na mkoa
(RCO) kwa kujihusisha na
mchezo mchafu wa
kuwabambikia kesi za
mauaji, kuchelewesha
upelelezi na kujihusisha na
ufisadi wa kutaka rushwa ili
wapeleleze haraka kesi zao.
Hata hivyo baada ya muda
mfupi, askari wa Magereza
waliamua kuondoa gari la
mahabusu hao mahakamani
na kuwarejesha gerezani
Kisongo, huku wao
wakikishangilia kwa nguvu
na kuendelea kuimba
nyimbo mbalimbali.
Akizungumzia madai ya
mahabusu hao, Msajili wa
Mahakama, Willbard
Mashauri, alisema madai ya
mahabusu hayo yanaweza
kuwa na ukweli ama
kutokuwa na ukweli, lakini
Mahakama haihusiki na
madai hayo na kueleza kuwa
Polisi na wapelelezi wa
makosa ya jinai ndio wenye
kulalamikiwa.
‘’Unajua kesi nyingi
zinazolalamikiwa na
mahabusu hao hazituhusu,
zinawahusu zaidi Polisi na
mwanasheria wa Serikali
ambaye ndiye mwenye
kuandaa mashitaka, sasa sisi
Mahakama tunahusikaje,‘’
alihoji Mashauri.
Alisisitiza kuwa pamoja na
mahakama kukabiliwa na
changamoto ya ukosefu wa
fedha za kuendeshea kesi za
mauaji, hivi sasa Mahakama
Kuu Kanda ya Arusha
imepata fedha za
kuendeshea kesi hizo.
Alisema majaji wanatarajia
kuanza mzunguko wa
kusikiliza kesi za mauaji
katika wilaya mbalimbali za
Kanda ya Kaskazini, hali
ambayo itapunguza
malalamiko kwa mahabusu
wanaokabiliwa na kesi za
mauaji.

No comments:

Post a Comment