Dar es Salaam. Msako wa wezi
wa kwenye Mashine za Kutolea
Fedha (ATM), umeanza kuzaa
matunda baada ya raia wa
Bulgaria kukamatwa akiiba
kwenye ATM ya Bank of Africa
(BOA), Tawi la Afrikana,
Kinondoni, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa za benki,
mtuhumiwa huyo ambaye
hakutajwa jina lake alikamatwa
baada ya kamera maalumu
zilizowekwa kwenye ATM za BOA,
kumtambua kuwa ni mwizi sugu
wa benki hiyo anayetafutwa.
Mmoja wa wafanyakazi wa benki
hiyo ambaye hakupenda kutajwa
jina kwa kuwa si msemaji,
alisema tukio hilo lilitokea jana
saa 12 asubuhi baada ya
mtuhumiwa huyo kuwekewa
mitambo maalumu ya kumnasa.
Alisema benki hiyo ilipelekewa
malalamiko na baadhi ya wateja
kwamba wakienda kutoa fedha
kwenye ATM wanakuta akaunti
zao hazina salio wakati
wanaamini zilikuwa na fedha.
Chanzo hicho cha habari kilidai
kuwa baada ya kupelekewa
malalamiko hayo, waliweka
mitambo maalumu ya
kuwawezesha walinzi wa
maeneo ya ATM za BOA kumbaini
mtu atakayetoa fedha kwa njia
ya wizi.
“Kama Benki tuliweka mtambo
maalumu na mtuhumiwa huyo
alionekana kwenye mtambo
wetu, hivyo tuliwaagiza walinzi
wetu watakapomwona mtu huyo
wamkamate haraka
sana,”alisema.
Alisema mtuhumiwa huyo alianza
mchezo huo kwa muda mrefu
ambapo kwa kutumia kadi za
ATM zisizojulikana idadi yake,
alikuwa anakwenda kwenye ATM
mbalimbali za benki hiyo na
kutoa fedha hadi Sh10 milioni.
Kuhusu tukio la jana, mmoja wa
walinzi wa BOA aliyejitambulisha
kwa jina moja la Frenky alisema
mtuhumiwa huyo alipofika
kwenye ATM hiyo aliingia na
kuchukua fedha ambazo
alizipeleka kwenye gari lake.
Frenky alisema baada ya
kupeleka fedha hizo, alirudi kwa
mara ya pili ili achukue fedha
nyingine ndipo walinzi hao
walimkamata na kumfunga
pingu.
“Huyu mtuhumiwa mwenye asili
ya Kiarabu alifika na gari lake saa
12 asubuhi, aliingia kwenye ATM
na kutoa fedha ambazo
hazikujulikana ni shilingi ngapi
na kuzipeleka kwenye gari lake,
baadaye alirejea tena kwa ajili ya
kutoa fedha zingine, wakati
anaingia ndipo alipokamatwa na
mlinzi aliyekuwa analinda hapo,”
alisema Frenky.
Kamanda wa Polisi Kinondoni,
Camilius Wambura alikiri kutokea
kwa tukio hilo na kusema kuwa
mtuhumiwa anashikiliwa na
jeshi hilo huku uchunguzi dhidi
yake ukiendelea.
“Ni kweli taarifa nimezipata,
mtuhumiwa amekamatwa, bado
hatujajua ni kiasi gani ambacho
ameiba kwa kutumia mtandao,
tunaendelea na uchunguzi,”
alisema Wambura.
Tukio kama hili lilishawahi
kutokea mkoani Mwanza
Februari 19 mwaka huu na Jeshi
la Polisi mkoani Mwanza kwa
kushirikiana na maofisa ya Benki
ya NMB liliwatia mbaroni watu
watatu ambao walidaiwa kuiba
kiasi cha Sh700 milioni kwa
nyakati tofauti.
No comments:
Post a Comment