Monday, August 5, 2013

WATANZANIA WAISHIO NJE WAASWA KULEA WATOTO WAO KITANZANIA

WATANZANIA waishio nchi
za nje wametakiwa kuwalea
watoto wao katika misingi
bora ya malezi yanayofuata
mila, desturi na utamaduni
wa Mtanzania unaojikita
katika unyenyekevu, upendo,
ushirikiano na kuheshimu
watu.
Mwito huo umetolewa hivi
karibuni na mke wa Rais,
Mama Salma Kikwete wakati
wa futari ya pamoja
iliyoandaliwa na chama cha
watanzania waishio
Botswana (ATB) mjini
Gaborone nchini humo.
Mama Kikwete alisema ni
vizuri watoto wawe na tabia
njema inayokubalika na jamii
ya kitanzania kuliko kulelewa
katika mazingira
yatakayowafanya wajue mila
na tamaduni za nchi zingine,
kwani nyumbani ni
nyumbani na ili waendane
na hilo ni lazima walelewe
kama wazazi wao
walivyolelewa.
“Ninawapongeza kwa kuwa
na umoja imara na wenye
nguvu na ushirikiano ambao
unawafanya kuwa kitu
kimoja na pale ambapo
jambo lolote linatokea liwe
zuri au baya mnaweza
kukabiliana nalo kwani
umoja ni nguvu na mahali
penye upendo chuki
hujitenga”, alisema Mama
Kikwete.
Alisema ni jambo la
kufurahisha kuona ndani ya
umoja huo kuna umoja wa
kinamama ambao lengo lao
ni kuwaweka watoto
pamoja na kuwafundisha
mila na utamaduni wa
mtanzania.
Aliomba wanawake ambao
hawajajiunga na umoja huo
wajiunge wajenge
mshikamano ambao ni
silaha kubwa ya watanzania.
Kwa upande wake Balozi wa
Tanzania nchini humo,
Radhia Mtengeti alisema
umoja huo ni wa kuigwa
kutokana na kuwa na fungu
la kusaidia Watanzania
wenye shida.
Pia kila mwaka wanafanya
ukaguzi wa hesabu zao za
fedha, jambo ambalo ni
nadra kufanyika katika
vyama vingine. Balozi
Mtengeti alisema,
“nimekuwa nikishirikiana na
umoja huu katika kazi zangu
zote ni watu
wanaoshirikiana na Serikali
na hata pale ambapo sipo
kazi zimekuwa zikifanyika
bila tatizo hakika najivunia
kuwa na watanzania wenye
moyo wa kujitolea na
kujituma kama hawa”.
Alisema wao kama
watanzania wanaoishi nje ya
nchi kwa njia moja au
nyingine wanaunga mkono
kuchangia mikakati
mbalimbali ya maendeleo ya
kuwasaidia watanzania,
kwani nchi yenye maendeleo
ya mama na mtoto ni lazima
itambulike kimataifa.
Mwenyekiti wa Umoja wa
akinamama, Rehema
Kalabam alimpongeza Mama
Kikwete kwa kazi kubwa
anayoifanya ya kuisaidia
jamii ili kuhakikisha kuwa
mama na watoto wa
Tanzania wanapata
maendeleo.
Alimuomba aendelee
kufanya hivyo kwa kuwa
akiwa mke wa Rais, akiamua
kufanya jambo kila mtu
atamsikiliza na kumuunga
mkono.
“Tuliamua kuanzisha umoja
huu tangu mwaka 2004,
lengo letu kuu likiwa ni
kuhakikisha kuwa akina
mama wanashiriki kikamilifu
katika kusaidia malezi ya
jamii na hasa watoto wa
kitanzania, kuwafundisha
mila na utamaduni mzuri wa
nyumbani na wa hapa
ambazo ni nzuri”, alisema
Kalabam.
Alisema wanawasaidia
vijana katika hatua za ukuaji,
kuwakutanisha wanawake
ili waweze kuangalia namna
wanavyoweza kuwasaidia
watu wenye mahitaji nchini
Botwana na Tanzania.
Mama Kikwete alikuwa
nchini akihudhuria mkutano
wa Kamati Maalumu ya
viongozi wanaoshughulikia
huduma na elimu ya afya ya
uzazi na jinsia kutoka nchi
za Jumuiya ya Afrika ya
Mashariki (EAC) na Jumuiya
ya Ushirikiano wa
Maendeleo ya Kikanda kwa
nchi za Kusini mwa Afrika
(SADC).

No comments:

Post a Comment