Monday, August 5, 2013

ROBERT MUGABE;MUHULA WA SABA NDANI YA IKULU HASARE

Harare. Baada ya kutangazwa
kuwa mshindi wa kinyan’ganyiro
cha Urais wa Zimbabwe, Rais
Robert Mugabe (89), amefikisha
mihula saba ndani ya Ikulu ya
nchi hiyo.
Mugabe juzi alishinda tena kiti
cha urais. Matokeo rasmi
yalionyesha kuwa aliibuka na
ushindi wa asilimia 61 wa kura
dhidi ya mpinzani wake,
aliyekuwa Waziri Mkuu, Morgan
Tsvangirai ambaye alipata
asilimia 34.
Chama cha Zanu-PF
kinachoongozwa na Mugabe na
kile cha MDC cha Tsvangirai,
viliunda Serikali ya Muungano
mwaka 2008.
Juzi, Tume ya Uchaguzi
Zimbabwe (ZEC), ilimtangaza
Mugabe kuwa mshindi katika
uchaguzi wa Rais uliofanyika
Jumatano iliyopita.
Zanu-PF pia kilipata ushindi
mkubwa katika uchaguzi wa
wabunge baada ya kujinyakulia
viti 137 kati ya 210.
Hata hivyo, inaelezwa kuwa hali
inaweza kuwa tete hasa baada
ya matokeo hayo ambayo
yalipingwa na Tsvangirai na
chama chake cha MDC.
Tsvangirai alisema Chama cha
MDC kitaisusia Serikali ya Mugabe
na kupinga matokeo ya uchaguzi
mahakamani. Wasimamizi wa
uchaguzi kutoka Umoja wa
Afrika wamesema uchaguzi huo
ulikuwa huru na wa haki.
Aidha, Jumuiya ya Maendeleo ya
Kusini mwa Afrika (SADC),
ilimtaka Tsvangirai akubali
matokeo ya uchaguzi.
Wasiwasi
Malalamiko yanayotolewa sasa na
wapinzani kuhusu uchaguzi huo
yanazidisha uwezekano wa
kuibuka machafuko kama
yaliyotokea 2008.
Mwaka huo, Tsvangirai aliongoza
katika duru ya kwanza ya
uchaguzi wa Rais na Zanu-PF
kilipinga ushindi huo. Ghasia na
machafuko vilitokea na
kusababisha kuuawa kwa mamia
ya wafuasi wa Tsvangirai.
Umwagaji damu uliotokana na
uchaguzi huo ulimfanya
Tsvangirai ajitoe kushiriki katika
duru ya pili ya uchaguzi na hivyo
kutoa mwanya kwa Mugabe
kutangazwa kuwa mshindi wa
duru hiyo kirahisi.
Hata hivyo, shinikizo la kimataifa
lililofuata, lilimlazimu Mugabe
kuunda Serikali ya umoja wa
kitaifa kwa kuishirikisha MDC.
Tayari wananchi wa Zimbabwe
katika Mji Mkuu wa Harare
wanaamini kwamba wanapaswa
kuheshimu matokeo ya uchaguzi
na kujiepusha na kuibuka kwa
machafuko.

No comments:

Post a Comment