WASICHANA sita wanaosoma
katika Shule ya Sekondari
Mzindakaya katika Kijiji cha
Kaengesa wilayani
Sumbawanga
wamenusurika kubakwa
baada ya mlango wa
nyumba yao kuvunjwa na
watu wasiofahamika na
kutishia kuwaingilia kimwili
kwa nguvu .
Wakisimulia kisa hicho
wasichana hao walimweleza
mwandishi wa habari hizi
aliyefika shuleni hapo juzi
kuwa ni baada ya wiki moja
tangu wenzao wawili
kubakwa kwa zamu na mtu
mmoja asiyefahamika
ambapo mwanafunzi mmoja
aliyekuwa akisoma kidato
cha nne shuleni hapo kati ya
hao waliobakwa alijiua kwa
kunywa sumu ya panya.
Kwa mujibu wa wanafunzi
hao watano kati ya sita
walidai tukio hilo lilitokea
usiku wa manane kuamkia
Alhamisi wiki hii ambapo
wote sita wakiwa wamelala
chumbani mwao
waligutushwa na sauti ya
mlango uliokuwa
umefunguliwa na watu
wawili waliokuwa wamevaa
‘kininja’ kuficha sura zao.
“Tulipogutuka tulianza
kupiga kelele kwa sauti ya
juu ndipo watu hao wawili
waliokuwa na kisu na rungu
walitumulika na kurunzi ya
mwanga mkali usoni. Bila
shaka waliacha kutubaka
walipobaini kuwa tulikuwa
wengi,” alisema mmoja wa
wanafunzi hao na kuongeza:
“Ndipo walipoanza kutupiga
kwa marungu
wakitulazimisha tuwapatie
fedha zote tulizokuwa nazo,
sisi tuliwaambia kuwa
hatuna chochote ndipo
walipozidi kutupiga marugu
mwilini na kutishia
kutuchoma kisu iwapo
tungejaribu tena kupiga
kelele za kuomba msaada”.
Kwa mujibu wa wanafunzi
hao ambao walikuwa
wamerejea kutibiwa katika
zahanati kijijini humo
walidai kuwa ndipo wenzao
wawili waliamua kutoa
akiba zao mmoja aliwapatia
Sh 1,300 na mwenzao
mwingine alikuwa na Sh 800
hivyo jumla walijikusanyia Sh
2,100.
“Lakini sisi ambao hatukuwa
na pesa yoyote ya kuwapatia
walizidi kutupiga marungu
bahati mbaya sana
walimpiga mwenzetu mmoja
ambaye alikuwa anaumwa
na kumwongezea maumivu
mwilini kisha wakatokomea
kusikojulikana, “ alisema
mmoja wao.
Wanafunzi hao watano kwa
pamoja walidai kufikia
maamuzi ya kuhama
nyumba hiyo ambapo
walikuwa kwenye mchakato
wa kupanga chumba katika
nyumba nyingine kijijini
humo.
Pia wamewalaumu wazazi
wao kwa kuwa wagumu
kuchangia ili waweze kuishi
katika hosteli za shule kwa
usalama wao. Hata hivyo
walimu na wanafunzi wa
shule hiyo wanawashuku
vijana waliovamia kwa wingi
kijijini hapo maarufu kama
‘wezi wa mafuta’
wanashirikiana na baadhi ya
wakazi wa kijiji hicho
kufanya vitendo vya kihalifu
kijijini hapo ikiwemo visa
vya ubakaji wa wanafunzi
wa shule hiyo waliopanga
vyumba kijijini humo.
Wakati mwandishi wa
habari hizi alipofika shuleni
hapo Mkuu wa Shule hiyo ,
Nicholas Thomas na walimu
wengine walikuwa
wanakutana na Ofisa Kata
wa Kaengesa kwa
mashauriano ya kuimarisha
usalama na ulinzi kijijini
humo.
Mkuu huyo wa Shule
alilieleza gazeti hili kuwa
mwanafunzi aliyekuwa
ameumizwa ametibiwa na
kuruhusiwa. Pia wazazi
wake wameridhia kuwa
kuanzia siku hiyo aanze
kuishi katika hosteli za shule
hiyo kwa usalama wake.
No comments:
Post a Comment